Saturday, 9 August 2014

MDUDU ALINIUMA






MDUDU ALINIUMA

Mbinguni,
jua lilikuwa limemaliza kazi yake na sasa lilijikokota magharibi huku
mionzi yake miekundu ikiwapungia walimwengu kwa ulegevu kana kwamba
kuwashukuru wale wote walioipenda. Masikini nilibaki pale uani
nimelitumbulia macho, huku machozi yakijikusanya tayari kumwagika. Heri
ningekuwa jua. Nisingekuwa na wasiwasi wa swala lolote. Langu lingekuwa
tu kuchomoza asubuhi na kutua jioni.
Nilikuwa nimechoka kuwatazama wapita njia na magari ya kifahari.
Yalikuwa mapya na yalikwenda kwa kasi tena bila kutoa sauti. Lakini kuna
yale yaliyochakaa yenye breki zilizokwaruzana kila yaliposimama. Watu
nao walipita wa aina tofautitofauti; si weusi, si weupe, warefu kwa
wafupi na hata vijana kwa wazee. Kwa umbali,taa za umeme zilikuwa
zimelimwaia jiji mchana bandia wa mwangaza. Ishara kuwa usiku ulikuwa
unaingia na giza kuanza kutawazwa.


Yote hayo sikuyaonea fahari tena. Mambo yalikuwa kangaja kumbe na
sasa yalikuja. Niliketi nikiwazia matokeo ya daktari, ambayo niliyapokea
takribani miezi miwili iliyopita. Awali, walinificha ukweli lakini
niliposisitiza, nilipasuliwa mbarika. Laiti wasingelinijuza kwani tangu
hapo maisha yangu yalichukua mkondo tofauti mno. Mwenyewe, ile hamu na
tama ya kula vyakula iliniondokea. Nikawa sili lolote, sinywi chochote.
Mashavu yangu yalizidi kushobwekea ajabu. Nguo zangu ningezivua, mbavu
zingehesabika hadharani moja baada ya nyingine. Nyele zangu zilizokuwa
ndefu na nyeusi ti sasa zilibadili rangi na kuanza kuchipuka ovyoovyo.
Mdudu alikuwa ameniuma. Lakini yupi?


Darubini yangu ilinikumbusha mambo yalivyoanza. Yote yaling’oa nanga
baada ya kumaliza kidato cha nne. ‘Mrembo’ nilijidai kwenda jijini
kutafuta kazi ya ukarani. Niliwahakikishia wazazi kuwa nilikuwa na
rafiki wengi waliojitolea kunipa makao wakati nikitafuta kazi. Wavyele
wakadinda kuniruhusu mwanzoni lakini baada ya kuzidi kusisitiza na
kufanya kiburi nyumbani, waliafikiana na kuniacha kwenda zangu. Pengine
walikumbuka kuwa mtoto akililia wembe mpe. Nilipokuwa nikiondoka, mama
alikuwa na huzuni mno na kwa uchungu, alinionya kuwa mwenda tezi na omo
marejeo ni ngamani. Potelea pote. Sikutaka kusikia ya yeyote kwani
nilijitia hamnazo nisikie la mwadhini wala la mteka maji msikitini.
Nikawa binti kiziwi asiyesikia anayoambiwa.


Kazi baada ya kuikosa,nilijiunga na wenzangu na tukajiajiri wenyewe.
Malipo yakawa ya kuvutia ajabu kwani wateja walivyoongezeka ndivyo
malipo yalivyoongezeka. Alimradi ujue namna ya kuwaongelesha na
kuwahudumia wateja sawasawa. Jambo ambalo nilijifunza kufanya hata
nikabobea na kutopea katika nyanja hiyo. Waume niliwabadili kama
nilivyobadili mavazi yangu kwa siku. Nikawa ndiye jogoo la shamba
lililowika jijini. Nikazika katika kaburi la sahau kuwa jijini kuna papa
na papaupanga, ambao ukiwapapia, hukosi kupapatika kwa majuto, dhiki na
mateso kama hayo yaliyonikumba sasa. Lau kumbe mwiba wa kujidunga hauna
kilio.


Kutoka hapo uani nilikoketi, taa za umeme nilizoziona zilinikumbusha
mengi. Kuhusu mienendo yangu ya awali nilipokuwa kipusa ajabu. Niliingia
kwa vilabu hivyo vyote vya usiku huku mikono ya watu tofauti yamezinga
kiuno changu chembamba kama cha nyigu. Daima kucha zangu zilizokuwa
ndefu na zilinaksishwa rangi sawia na nguo zilizovalika.  Mdomo wangu
ukakolezwa rangi nyekundu kana kwamba nililamba damu mbichi. Lakini
kumbe dunia mti makavu kiumbe usiuegemee.


Watu hao niliowatazama waliniongezea uchungu mtupu. Moyo wangu
mchanga ulijaa uchukivu na furaha ikawa imeyeyuka kama kipande barafu
katika utupu wa mchanga wa jangwa la Sahara. Wale wasichana warembo
waliovalia mavazi yaliyoacha sehemu za miiliyao kuonekana waliniudhi
zaidi. Laiti wangelijua kuwa dunia itawararua na kuwaacha uchiuchi,
wasingefika hata barabarani. Nilitamani kuwafikia niwaonye na kuwapa
ukweli wa mambo kuhusu madhara ambayo yangewasibu lakini nilishindwa.
Mimi pia nilikuwa hivyo na sasa nilikuwa naangamia. Nikakumbuka kuwa
asiyefunzwa na mamake hufunzwa na ulimwengu.


Waume nao niliwatazama kama wanyama mwitu waliovalia suruali ndefu na
sharti tofauti. Wanyama wenye uwezo mkali wa kukuvamia wakakumaliza
kabisa. Wao ndio walionipa maji machafu yaliyokuwa na mdudu ambaye
aliniuma na kunifanya kuugua sasa. Niliwatazama kwa uchukivu mwingi.


Raha nyingi ya ulimwengu ulitoweka na badala yake ikawa sasa ni
huzuni tupu na majuto. Sasa niliishi kwa jumba hilo kubwa peke yangu.
Ulimwengu ulinitenga kana kwamba mwenye ukoma. Wale wote waliokuwa
wakiingia na kutoka siku nzima hata usingewaona. Dada yangu mdogo ndiye
alijitolea kuniuguza pale kwani sikutaka kuishi na wazazi na kuwapa
mzigo wa kunitunza. Ikanijia kuwa mla nawe hafi nawe ila mzaliwa nawe.
Sikujua wa kumlaumu. Wazazi? La wao walinitakia mema na kunionya kusoma
kwa bidii. Marafiki? Kwa kiasi kidogo lakini ndimi niliyekubali
kudanganywa. Ulimwengu? Ndiyo lakini sehemu gani ya ulimwengu? Mimi
ndiye wakulaumu na sasa mwiba wa kujidunga hauna kilio.


Ndoto zangu zote zilitoeka kama ukungu na umande. Azimio langu la
kutaka kuendeleza masomo katika chuo kikuu katika fani ya sheria, na
kufuzu katika uzamifu na uzamili lilitoweka ghafla kama mwangaza wa
mshumaa uliozimwa na upepo. Nilitoka uani na kuingia katika chumba
changu cha kulala. Mezani, kulikuwa picha yangu ya awali.nilijiangalia
tena na kujiona tofauti; mnene, mwenye sura ya maji ya kunde tena
mcheshi ajabu. Lakini sasa nilikuwa kama shetani hata ingawa sijawahi
kuonana naye ana kwa ana. Haina maana kuishi katika hali hiyo!
Niliifikia kalamu na kuandika kitu kwa karatasi iliyokuwa hapo kando.
Kasha nikavuta kijichupa kilichokuwa hapo juu na kupiga makopo kadhaa ya
yaliyokuwemo. Maini ya kaanza kukeketeka na koo kuungua ndanindani.
Heri nife niiondokee dunia. Safari yangu ya kuenda jongomeoni ikawa
imeanza nilikolala sakafuni.


Niligutuka usingizini nikihema na kutweta kwa nguvu mno hata nikashindwa kuendelea kulala. Ilikuwa ndoto ya ajabu.


MAUTI YALIBISHA MLANGONI


MAUTI YALIBISHA MLANGONImauti yalibisha

Daktari
Mogiri alifungua mlango polepole na kutoka nje. Alinikuta nimeketi kwa
fomu ndefu hapo nje ya wodi nikisubiri. Nilikuwa nimejishika tama na
kuzama katika luja ya mawazo. Ni kweli kwamba mshika tama huwa analo
moyoni.nilimwangalia kwa macho ya atiati nikitazamiakusikia mengi
kumhusu mke wangu Zuhura. Sikujua kilichomtendekea tangu aingizwe mle
ndani ya chumba cha upasuaji, masaa matano yaliyopita. Kumbe kweli
usilolijua ni kama usiku wa manane.


Akilini mwangu, yaliyotendeka yalikuwa yangali mbichi mno. Nilitoka
kazini mapema alasiri hiyo na kurudi nyumbani kwani sikuwa na kazi
nyingi ya kufanya. Nikafululiza hadi mlangoni na kubisha bila kupata
jibu.wanenao husema kuwa kimya kingi kina mshindo. Nilifungua mlango
polepole na kuingia ili kugundua kilichonisubiri. Lo! Ukistaajabu ya
musa utayaona ya firauni.


Zuhura alikuwa kalala sakafuni, akigaaga na kufurukuta kwa uchungu na
kutoa sauti ya maumivu. Aliye na macho haambiwi tazama. Nilielewa fika
kuwasiku zake za kujifungua zilikuwa zimewadia. Kasha akajikazana
kutamka,


“Nisaidie jamani.” Kisha akanyamaa ghafla na kuendelea kufurukuta.
Fimbo ya mbali haiui nyoki kwa hivyo, niliwaita majirani walionipa
usaidizi wa kutafuta rukwama ili kumpeleka hospitalini. Ilikuwa nadra na
adimu kama wali wa daku kuona magari katika sehemu tuliyoishi. Sehemu
ya Ngomani. Kama wakaazi wa pale, tulizoea maisha hayo na haikuwa ajabu
kumwona akipanda au kuabiri ‘gari’ letu- rukwama. tulimpeleka kwa
zahanati ya kipekee hapo mjini na kupata kuwa muuguzi hakuwepo. Nikawa
nimechanganyikiwa nisijue la kufanya  jirani mmoja aliposhauri
tumkimbize Zuhura katika hospitali ya wilaya.


Hospitali ya Afueni ilijulikana kote kwa kuwa ya bei ghali. Lakini
nilishawishika na kukubali kwani maisha ya Zuhura ilikuwa muhimu kuliko
pesa. Tukaandamana hadi kule. Hisia za uchovu na kutamauka tayari
zilianza kuninyemelea nikawa nafuata wenzangu tu kama bendera
inavyofuata upepo au maji inavyofuata mkondo. Moyo wangu ulijaa ukunjufu
kwa ukarimu walionionyesha.


Nikawa
nimeketi hapo nikisubiri matokeo ya daktari waliokuwa wakimhudumia.
Takribani miaka mine sasa tangu tufunge ndoa, Zuhura alibaki tasa
asiweze kupata motto hata mmoja. Mara nyingi nilimsikia akimlilia Muumba
wake na kusali. Hatimaye maombi yake yalijibiwa na sasa tulikuwa
tukitarajia mwana wetu wa kwanza. Tayari nilikuwa na cheche za
matumaini. Penye nia pana njia eti. Hata nikakisia kuwa atakuwa msichana
na tungemwita Zawadi. Pengine kama ishara kuwa Maulana alitupa zawadi
baada ya miaka. Nilisahau kabisa onyo la wahenga eti usikate kanzu kabla
motto hajazaliwa.


Daktari Mogiri akanisongelea na tukaanza majadiliano. Mazungumzo ya
kiume kama alivyoyataja. Mara kwa mara niliwaona wauguzi wakipitapita
kushoto-kulia wakiendelea na shughuli zao. Daktari alikuwa amemaliza
kazi yake muhimu mle ndani.


“Unatarajia mtoto wa jinsia ipi? Mbona? Mtamwita nani? Utampa Zuhura
zawadi gain kwa kazi aliyofanya?” aliniuliza maswali chungu nzima.
Maswali yenyewe yakatuongoza katika ulimwengu wa gumzo. Tukazungumza na
kupitiza wakati bila hata kugundua. Hata chembechembe za wasiwasi
nilizokuwa nazo zikanitoka kabisa. Nikajihisi huru, kiumbe mpya na
nikavaa piku la tabasamu.


Ndipo sasa daktari akaamua kunipasulia mbarika hatimaye. Akanidokezea
kuwa  Zuhura alikuwa amejifungua motto wa kiume mwenye buheri wa afya.
Singejizuia tena.licha ya kuwa
usiku ulikuwa umeingia, nilirukaruka kwa furaha kupindukia ungedhani
mwenda wazimu. Nikatamani majirani wote waliomleta Zuhura wangalikuwepo
lakini walikuwa washarudi makwao kushughulikia jamii zao.       Nikaanza
kuwazia jina la motto wetu nikiwa katika hali ya kurukaruka
bado.                                           “Tutamwita Bahati”
Nilisema kwa nguvu huku nimemkumbatia daktari kwa furaha macho yangu
nikiwa nimeyafumba.


Daktari alikuwa akinitazama tu kwa wakati wote huo pasi na la kusema.
Lakini nilipoanza kuuelekea mlango wa chumba alimolazwa mke wangu,
alinisitisha na kunizuia. Akaniomba kusubiri lakini furaha iliyonijaa
ikanifanya kuwa kiziwi. Nikajitia pamba masikioni nisisikie la mwadhini
wala la mteka maji msikitini.


Akanivuta kando kidogo na kunidokezea kuwa Zuhura mwenyewe alifuja na
kupoteza damu nyingi hivyo basi asingeweza kuishi! Kwa kifupi,
aliniambia kuwa mke wangu alikuwa amea…sikuyaamini macho na masikio
yangu. Maneno hayo yalinifanya kiuwa chakaramu zaidi. Yalinikata maini,
yakanikera na kunikereketa ajabu. Uso wangu uliokuwa na furaha
ulibadilika ghafla na kufinga. Kwa nguvu kama za tembo na hasira za
mkizi, niliuendea ule mlango bila kumjali yeyote wala chochote.
Alinifuata na kujaribu kunivuta nyuma huku akiniliwaza. Juhudi zake
zikangonga mwamba.


Sikujua kuwa daktari ni watu wenye vipawa vha kuwapumbaza watu namna
hiyo! Kwa muda wote huo, daktari alikuwa amejua ukweli na kunificha kwa
kunishirikisha katika mazungumzo. Pengine hayo ni baadhi ya mafunzo
wanayopewa wanaposomea fani ya udaktari lakini ubunifu wa ya Mogiri
ulishinda wote. Niliajabia ubunifu wake!


Niliingia kwa fujo na rabsha kama mfungwa aliyeachiliwa huru. Wauguzi
wakashtuka na kujaribu kunizuia. Daktari akaingia na kuagiza nionyeshwe
mtoto. Nikaelekezwa hadi alikokuwa. Mtanashati ajabu na mwenye afya
ungedhani kutoka mbinguni. Alilala kwa utulivu asijue mamake alikokuwa.
Laiti angejua. Lakini kuonyeshwa mtoto haikunisaidia wala kinutuliza.
Nani angekilisha,akivishe na kukilinda siku zote? Unyama upi huo
kuingizwa katika ulimwengu na kuachwa na mwenyeji wako hata kabla ya
kumwona ana kwa ana? Nilijihurumia, nikamhurumia malaika wa Mungu.
Machozi yakanidondoka kama mtoto na nikayaacha kumwagika bila aibu.


Kwa mwongozo wa daktari, nilifululiza hadi alikolazwa Zuhura.
Msichana mrembo aliyeumbwa akaumbika alikuwa amelala kwa upole na
utulivu asijue hata wakati wa kuamka. Alikuwa amefunikwa vizuri hata
usingedhani ni maiti. Ikanifanya kutoamini na kuanza kumwamsha. “Zuhura,
amka umwone Bahati mwana wetu.”


Akawa haoni, hasemezi,hatikisiki. Kimya kikajiri. Niliinama  kando
yake na kumtikisa tena mara hii kwa nguvu machozi zaidi yakinitoka.
Nikamshauri ainuke twende kwetu tusherehekee kuzaliwa kwa mtoto wetu.
“Zuhura” niliita mara ya mwisho kwa nguvu na pumzi ikaniishia.


Sauti nyororo ya Zuhura aliyekuwa amelala kando yangu usiku wote
ilinigutusha kutoka usingizini ikinijuza kuwa kumekucha. Miale ya jua
nayo ilikuwa imeshachomoza nje. Furaha iliyoje kupata kuwa hiyo ilikuwa
ndoto ya ajabu.


Tuesday, 29 July 2014

INSHA MUFTI AND AWESOME COMPOSITION: JINSI YA KUANDIKA INSHA MUFTI

INSHA MUFTI AND AWESOME COMPOSITION: JINSI YA KUANDIKA INSHA MUFTI




Miaka Kumi Baadaye, Nakukumbuka Babangu!

Tarehe kamili kama leo miaka kumi iliyopita, jambo lililobadili maisha yangu
kabisa lilitokea. Asubuhi Desemba tarehe 2 2001, nilijinyanyua kwenda
kufunga mfereji wa maji uliyokuwa ukichuruzika usiku kucha. Baba alikuwa
amenikumbusha kuufunga vyema kabla kulala ili maji yatakapofunguliwa
usiku katika bomba kuu la jengo letu, yasipate kumwagika. Ni agizo
ambalo nilisahau kutimiza na hivyo kulazimika kuamka alfajiri na mapema
saa kumi na moja kwenda kuzima. Kibaridi kisicho cha kawaida kilinipiga
mwilini na kunifanya kuganda. Nilihisi kuwa kuna jambo lisilo la kawaida
linalonitendekea lakini sikujua ni wapi au vipi.


Nilihofia manake nilidhani nitampata baba ameamka kama ilivyokuwa
desturi yake ili ajitayarishe kwenda kazini. Laiti ningalijuwa
yaliyonisubiri! Nikakwenda mlangoni mwa chumba alimolala baba na kubisha
mlango kwa upole. Baba! Baba! Baba! Niliitana lakini sikupata jawabu.
Jambo ambalo halikuwa la kawaida.


Kwa utaratibu mkubwa niiliiufungua mlango na kuingia. Nikanyatia
kitandani alikolala baba na kuanza kumtikisa huku nikimwita. Niliona
kuwa alikuwa amechelewa kuamka ili kujitayarisha kuenda kazini na iwapo
angeendelea kulala hivyo basi angechelewa kufika kazini.


“Baba! Amka baba wakati umefika” masikini niliitana nisipate jibu.
Jambo lililonipa msukumo wa kumfunua. Lo! Baba alikuwa amelala kwa
utulivu na kuunyosha mwili wake kabisa. Alikuwa kasha lala usingizi
usiojuwa wakati wake wa kuamka. Kama mchezo tena kwa ghafla, babangu
mzazi alikuwa ameaga katika usingizi wake. Niliona dunia yangu
ikizunguka na macho karibu yanitoke maanake sikujua pa kuanzia. Asubuhi
na mapema vile, na umri wangu mdogo wa miaka kumi na mitatu  tena katika
darasa la saba, ningeanzia wapi ilhali familia yetu ilikuwa katika mji
tofauti na mimi ndiye niliishi na baba? Ilikuwa mwaka wa 2001.
Yaliyofuatia yalibaki kitendawili kwani sikuwahi amini ya kuwa baba
yangu alikuwa ameaga hadi mwaka wa 2005!


Sasa
napiga darubini yangu nyuma, mengi yamejiri mno katika familia yetu
ambayo sina budi kumshukuru Maulana kwa majaliwa yake. Ndiye Mungu
mwenye kutujalia neema ndogondogo na neema kubwa kubwa. Babangu
akifufuka leo, atashtuka kumpata mwanawe wa kwanza alijitaidi masomoni
hadi kukamilisha chuo kikuu na kwa sasa ninachapa kazi! Ajabu maanake
aliniwacha katika darasa la saba wakati hata masomo ya msingi sikuwa
nimemaliza.  Wenzangu wanaonifuata pia wamejitahidi na kuingia katika
vyuo vikuu na wengine kukamilisha masomo ya sekondari.


Zaidi ya  yote, daima namshukuru mamangu mzazi. Amekuwa kipa imara
kwetu katika miaka hizi zote na kutia bidii kama za mchwa kuwapa wanawe
maisha bora. Isingalikuwa mamangu, nisingelikuwa nilipo. Amekuwa mnara
wetu nyakati zote! Alinipa tabasamu na sababu ya kuona siku mpya hata
nilipodhani kuwa yote yamekwisha.


Saturday, 31 May 2014

INSHA MUFTI AND AWESOME COMPOSITION: JINSI YA KUANDIKA INSHA MUFTI

INSHA MUFTI AND AWESOME COMPOSITION: JINSI YA KUANDIKA INSHA MUFTI

Kwa wapenzi wangu wote wa blogu hii zidi kutegea mengi kutoka kwa chungu hiki kilichokolea asali iliyo tamu na itakayokuwacha ukiviramba viwiko. Naunganisha timu yangu ili kukupa uhalisi wa ulichotarajia. Kwa ufupi, blogu bora wala si bora blogu